Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Wakili Albert Msando, amesema wamefanikisha kujenga mabanda mapya ya wafanyabiashara zaidi ya 200 katika Soko la Mawasiliano (Simu 2000) ikiwa zimepita wiki tatu tu tangu soko hilo liungue moto.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Msando amesema, “Hapa nipo Soko la Mawasiliano (Simu 2000). Soko letu baada ya kuungua tulipewa maelekezo na Rais, kwanza tuchunguze lakini pili tuhakikishe wafanyabiashara wanarejea katika hali ya kawaida wakiwa wanaendelea na biashara zao.”
Amesema ndani ya muda huo mfupi, serikali imefanikiwa kusafisha eneo na kujenga zaidi ya mabanda 200, hatua aliyosema imewezesha wafanyabiashara kurejea haraka kazini.
“Tumesafisha eneo kwa wakati na tumejenga mabanda mapya zaidi ya 200 kwa ajili ya wafanyabiashara hawa. Ndani ya wiki tatu tumewarejesha wafanyabiashara,” amesema.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa viongozi mbalimbali wa serikali, akiwemo Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa TAMISEMI na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Moto mkubwa uliteketeza soko hilo Aprili 4, 2026, na kuharibu zaidi ya mabanda 500 ya wafanyabiashara wadogo, ukiacha mamia yao bila mitaji wala sehemu ya kufanyia biashara.
Moto huo ulisambaa kwa kasi kutokana na miundombinu ya muda ya mabanda, huku chanzo chake kikiwa hakijathibitishwa rasmi, na kusababisha taharuki pamoja na hasara kubwa kiuchumi kwa wafanyabiashara na Halmashauri ya Ubungo.










