Msanii mkongwe wa filamu nchini, Hashim Kambi, amefariki dunia Aprili 27, 2026, baada ya kuzidiwa ghafla akiwa kazini jijini Dar es Salaam.
Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na msemaji wa Shirikisho la Filamu nchini, Coletha Raymond, aliyesema msanii huyo alianguka akiwa kazini muda mfupi baada ya kurejea kutoka Tabora.
“Ni kama dakika 30 hadi 40 zilizopita. Alikuwa ametokea Tabora kikazi na aliporejea akaelekea moja kwa moja kwenye kazi nyingine eneo la Pilipili, ndipo alipohisi hali siyo nzuri na kuzidiwa,” amesema.
Kambi alikimbizwa hospitali kwa matibabu, lakini alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa.
Kwa mujibu wa Raymond, msanii huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya presha pamoja na kisukari, hali inayodaiwa kuchangia kifo chake.
Ameongeza kuwa Shirikisho linaendelea na taratibu za ndani, ikiwa ni pamoja na kuitisha kikao kwa ajili ya kuanza mipango ya mazishi.
Kambi alikuwa miongoni mwa wasanii waliodumu kwa muda mrefu katika tasnia ya filamu Tanzania, akijijengea jina kupitia ushiriki wake katika filamu na tamthilia mbalimbali za Kiswahili.
Katika miaka ya hivi karibuni, alibaki kuwa hai katika tasnia hiyo, akiendelea kushiriki kazi za uigizaji na kushirikiana na kizazi kipya cha wasanii licha ya changamoto za kiafya.
Kifo chake kinaongeza orodha ya wasanii wakongwe waliowahi kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa tasnia ya filamu nchini, hasa katika kipindi cha kupanuka kwa filamu za Bongo Movie mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Tasnia ya burudani nchini inaendelea kukumbana na mjadala kuhusu ustawi wa wasanii wakongwe, wengi wao wakiendelea kufanya kazi bila mifumo imara ya afya au msaada wa kifedha.
Mahojiano yake ya mwisho na mwandishi wa habari mkongwe Sudi Mnete, yaliyofanyika Machi 12, 2026, Ubungo jijini Dar es Salaam, yalitoa mwanga juu ya safari yake kabla ya umaarufu wa filamu.
Katika mahojiano hayo, Hashim Kambi alieleza kuwa alianza kucheza soka miaka ya 1970 akiwa na timu ya Tumbaku mkoani Morogoro, kabla ya kujiunga na Klabu ya Yanga. Alisema alipata ajira yake ya kwanza alipokuwa kidato cha nne, akichanganya kazi na soka, hali iliyomfungulia mlango wa kucheza Yanga kama beki namba nne au tano.
Baada ya kuachana na soka, Kambi alipata shauku ya kuingia kwenye uigizaji. Alianza kwa majaribio madogo kabla ya kujipata kikamilifu katika tasnia hiyo, ambapo baadaye alipata umaarufu mkubwa kupitia filamu za ndani.










