Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi mpya za kuandikishwa kwa vijana wa Kitanzania, likieleza sifa, utaratibu wa maombi na muda wa kuwasilisha.
Tangazo hilo limetolewa na Kevin Baraka Byabato, Luteni Kanali na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya jeshi, Byabato amesema nafasi hizo zinawahusu vijana kuanzia wenye elimu ya sekondari hadi elimu ya juu, huku waliopata nafasi wakitarajiwa kupatiwa mafunzo ya kijeshi pamoja na mafunzo ya kuwaendeleza kitaaluma.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, waombaji wanapaswa kuwa raia wa Tanzania wa kuzaliwa, wenye umri usiozidi miaka 25 kwa waliomaliza kidato cha nne au sita, na miaka 28 kwa wenye elimu ya juu. Pia wanatakiwa kuwa na afya njema, akili timamu, nidhamu nzuri, na wasiwe na rekodi ya makosa ya jinai.
Jeshi pia limeweka masharti ya nyaraka, likihitaji waombaji kuwasilisha nakala ya kitambulisho cha taifa au namba ya NIDA, cheti cha kuzaliwa, vyeti vya elimu, pamoja na namba ya simu ya mkononi. Kwa wale waliopitia mafunzo ya JKT, wanapaswa kuambatanisha cheti kinachoonyesha wamemaliza mkataba wa kujitolea.
Aidha, tangazo hilo limeeleza wazi kuwa vijana waliopo kwenye makambi ya JKT kwa sasa hawahusiki na mchakato huu, huku wale waliowahi kuhudumu katika vyombo vingine vya ulinzi na usalama nao wakizuiwa kuomba.
Maombi yote yanatakiwa kuandikwa kwa mkono na kuwasilishwa kwa njia ya posta kwa Mkuu wa Utumishi Jeshini, Makao Makuu ya Jeshi, Sanduku la Posta 194, Dodoma.
Mchakato wa kupokea maombi unaanza Aprili 15, 2026 na utahitimishwa Aprili 28, 2026, muda ambao waombaji wanatakiwa kuhakikisha nyaraka zao zimewasilishwa kwa wakati.









