Mamlaka za Kenya zimemkamata raia wa China katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta baada ya kudaiwa kujaribu kusafirisha maelfu ya mchwa nje aina ya Queen Garden kinyume cha sheria za nchi.
Mshukiwa huyo aliyetambulika kwa jina la Zhang Kequn alikamatwa wakati wa ukaguzi wa kawaida wa usalama uwanjani hapo kabla ya safari yake kuelekea China.
Maafisa wa usalama waligundua mchwa zaidi ya 2,000 wakiwa wamehifadhiwa ndani ya vyombo vidogo vilivyokuwa vimefichwa kwenye mizigo yake.
Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi, mchwa hao walikuwa wamewekwa kwenye mirija midogo na vifaa maalumu vinavyotumika kuwahifadhi wakiwa hai wakati wa usafirishaji.
Mamlaka za wanyamapori nchini Kenya zinaamini kuwa mchwa hao walikuwa wakisafirishwa kwa ajili ya soko la kimataifa la wakusanyaji wa wadudu adimu na watafiti wa kisayansi.
Kesi hiyo imeibua wasiwasi miongoni mwa maafisa wa uhifadhi wa mazingira kuhusu ongezeko la biashara haramu ya viumbe hai wadogo kama wadudu, ambayo imeanza kushika kasi katika miaka ya hivi karibuni.
Mshukiwa huyo alifikishwa mahakamani huku mahakama ikiruhusu mamlaka za uchunguzi kuendelea kuchunguza vifaa vyake vya kielektroniki ikiwemo simu na kompyuta ili kubaini kama kuna washirika wengine katika mtandao huo.








