Mahakama Tanzania Yaamuru Kufungwa kwa Kampuni ya Sahara Media Group

Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara imeamuru kufungwa rasmi kwa kampuni ya Sahara Media Group Limited wamiliki wa Star Tv, Kiss FM pamoja na Radio Free Africa baada ya kubainika kuwa haina uwezo wa kuendelea na shughuli zake kutokana na matatizo makubwa ya kifedha.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Dkt. Mwajuma Kadilu baada ya mahakama kupokea maombi kutoka kwa kampuni hiyo yakieleza hali mbaya ya kifedha inayokabili biashara hiyo.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizowasilishwa mahakamani na Afisa Mkuu wa kampuni hiyo, Steven Diallo, Sahara Media Group ilipata hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 3.9 mwaka 2023 pekee.

Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa kampuni hiyo ina deni la takribani shilingi milioni 97.7 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na kodi ambazo hazijalipwa.

Ushahidi uliotolewa mahakamani ulionyesha kuwa sehemu kubwa ya mapato ya kampuni hiyo ilikuwa inaelekezwa kulipa madeni ya kodi, jambo lililoathiri uwezo wake wa kuendesha shughuli za kila siku ikiwemo uendeshaji wa vyombo vyake vya habari.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Kadilu alisema kuwa kutokana na hali hiyo ya kifedha, kufungwa kwa kampuni hiyo ni hatua sahihi ya kisheria ili kulinda maslahi ya wadai.

Mahakama ilimteua Wakili Alex Mgongolwa pamoja na Wakili Frank Mwalongo kusimamia mchakato wa kufilisi mali za kampuni hiyo.

Kazi yao itahusisha kusimamia mali za kampuni, kupokea madai ya wadai na kuratibu ulipaji wa madeni kwa mujibu wa sheria, huku mchakato huo ukitarajiwa kuchukua takribani miezi mitatu.

READ  Rais Mahama Awasili Tanzania kwa Maadhimisho ya Miaka 20 ya Mahakama ya Afrika