Mfanyabiashara mmoja kutoka Scotland (Uskochi) amepatikana akiwa ameuawa nchini Kenya, mwili wake ukiwa umefungwa na kuwekwa ndani ya gunia, huku polisi wakiwakamata watuhumiwa wanne katika tukio linalodaiwa kuwa ujambazi uliogeuka mauaji.
Marehemu aliyetambuliwa kama Campbell Scott alikuwa amesafiri kwenda Nairobi kuhudhuria mkutano wa kibiashara kabla ya kupotea. Mwili wake ulipatikana baadaye ukiwa umetupwa katika eneo la mbali, zaidi ya kilomita 100 kutoka jijini humo.
Wapelelezi wa Kenya wanasema Scott alitegwa kutoka katika klabu ya usiku na kupelekwa kwenye nyumba katika eneo la Pipeline, ambako alishikiliwa kwa saa kadhaa. Inaaminika washambuliaji walimfunga na kujaribu kumlazimisha kutoa taarifa za akaunti zake za benki, huku wakitumia kadi zake kufanya miamala katika maeneo tofauti.
Mamlaka zinasema tukio hilo lilikuwa sehemu ya mtandao mpana wa uhalifu unaolenga wageni kwa nia ya kujipatia fedha, lakini mambo yalizidi na kusababisha kifo chake. Baadaye mwili wake ulisafirishwa na kutupwa ndani ya gunia, ukiwa umefungwa mikono.
Polisi wamewakamata watuhumiwa wanne waliotambuliwa kama; Bernard Mbusu, Isaac Kinoti Kobia, Evans Muthengi Mutaki na Kelvin Mwangi Njoroge kufuatia operesheni ya kijasusi iliyofuatilia mienendo yao kati ya Nairobi na maeneo ya pwani.
Kukamatwa kwao kulifanyika wakati wa uchunguzi mpana wa matukio ya ujambazi wa kutumia nguvu, ambapo maafisa waliwaunganisha na mauaji hayo kupitia miamala ya benki, data za simu pamoja na vitu vilivyopatikana kama fedha za kigeni, simu na kadi za benki.
Maafisa wanasema kundi hilo linahusishwa na mtandao unaolenga wageni, jambo linalozua wasiwasi mpya kuhusu uhalifu wa kupangwa katika maeneo ya mijini.
Watuhumiwa hao bado wanashikiliwa huku uchunguzi ukiendelea, na mamlaka zikisema huenda watu wengine zaidi wakakamatwa kadri wanavyoendelea kufichua mtandao huo.








