Mastodon

Mwanamke Tanzania ashikiliwa kwa tuhuma za kumuua mumewe kwa panga

Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 50, anayefahamika kwa jina la Maselina Mtewele, anashikiliwa na polisi mkoani Njombe kwa tuhuma za kumuua mumewe, Gwido Kigaya (59), kwa kumkata kwa panga kichwani.

Tukio hilo lilitokea Machi 18, 2026 majira ya saa saba usiku katika kijiji cha Lwangu, baada ya kile kinachodaiwa kuwa ugomvi wa muda mrefu kati ya wanandoa hao.

Mashuhuda, akiwemo Magnus Mayemba na Albentina Mayemba, wanasema wawili hao walikuwa wakigombana mara kwa mara, na siku ya tukio walikuwa wakigombania jembe kabla hali haijageuka kuwa vurugu.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alichukua panga na kumshambulia mumewe, tukio lililosababisha majeraha makubwa kichwani yaliyosababisha kifo chake.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Johnbosco Kigae, amesema kuwa kabla ya tukio hilo, tayari kulikuwa na historia ya migogoro ya kifamilia kati ya wawili hao.

“Walikuwa wakitengana mara kwa mara. Kila mmoja aliishi kivyake, hata huduma za ndoa zilikuwa hazipo,” amesema Kigae.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, amethibitisha tukio hilo na kusema mtuhumiwa yupo chini ya ulinzi huku uchunguzi ukiendelea.

READ  Mahakama Tanzania Yaamuru Kufungwa kwa Kampuni ya Sahara Media Group