Meli kadhaa za kubeba magari zimeanza kubadili safari na kuelekea Bandari ya Lamu nchini Kenya, kufuatia kuongezeka kwa hatari za usalama katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Hatua hiyo imeathiri moja kwa moja usafirishaji wa kimataifa, huku angalau meli tatu zikiripotiwa kufika Lamu baada ya kushindwa kuendelea na safari kuelekea Mashariki ya Kati.
Moja ya meli hizo, iliyokuwa imebeba takribani magari 3,800 kutoka Yokohama, Japan kuelekea Jebel Ali, ililazimika kushusha mzigo wake Lamu baada ya njia hiyo kuwa hatarishi.
Mgogoro unaoendelea katika eneo la Hormuz umeifanya njia hiyo kuwa hatari kwa meli za biashara, huku mashambulizi dhidi ya meli na vitisho vya kijeshi vikiongeza hofu kwa wasafirishaji.
Kwa kawaida, takribani asilimia 20 ya mafuta ya dunia hupita katika mlango huo wa bahari, lakini sasa usafiri umepungua kwa kiasi kikubwa huku baadhi ya meli zikisimamishwa au kubadili njia kabisa.
Kutokana na hali hiyo, bandari za Afrika Mashariki kama Lamu na Mombasa zimeanza kupokea ongezeko la meli, zikichukua nafasi kama njia mbadala ya biashara ya kimataifa.
Ripoti zinaonyesha kuwa maelfu ya magari, pamoja na mizigo mingine, sasa yamekwama au yanahifadhiwa kwa muda katika bandari hizo wakati wamiliki wakitafuta njia mpya za kuyafikisha katika masoko yaliyokusudiwa.
Wachambuzi wa sekta ya usafirishaji wanasema mabadiliko hayo yanaweza kuifanya Lamu kuwa kitovu kipya cha muda katika biashara ya ukanda wa Afrika Mashariki, hasa wakati mgogoro wa Mashariki ya Kati ukiendelea kuathiri njia kuu za baharini.







