Mahakama ya Iringa yahukumu dereva bajaji kunyongwa kwa kumuua mwanawe wa miaka minne kisa utajiri

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, imemhukumu kunyongwa hadi kufa Joseph Yustino Muhulila (28) baada ya kumkuta na hatia ya kumuua mwanawe, Timotheo Joseph, mwenye umri wa miaka minne.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Angaza Mwipopo katika kesi namba 25532 ya mwaka 2025, ambapo mahakama ilieleza kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi uliothibitisha kosa bila kuacha shaka kwa mujibu wa vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama, tukio hilo lilitokea kati ya Aprili 9 na 12, 2025 katika Kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa. Ilielezwa kuwa mshtakiwa alimshawishi mtoto huyo kabla ya kumuua, kisha akaukata mwili vipande na kutupa mabaki kwenye choo cha shimo na tenki la maji.

Mahakama ilisikia kuwa mshtakiwa alijaribu kuficha tukio hilo kwa kutoa taarifa za kupotosha kwa polisi, akidai awali kuwa mtoto alikuwa amepotea katika mazingira yasiyoeleweka.

Ushahidi uliowasilishwa ulijumuisha uchunguzi wa vinasaba (DNA) uliothibitisha kwa asilimia 99 kuwa mabaki yaliyopatikana yalikuwa ya mtoto huyo na yalikuwa na uhusiano wa kibaolojia na mshtakiwa.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha mashahidi 13, ambao ushahidi wao uliisaidia mahakama kuunganisha mlolongo wa matukio hadi kufikia mauaji na utupaji wa mwili.

Katika mwenendo wa kesi, mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo, akieleza kuwa alifanya hivyo kwa lengo la kupata fedha. Mahakama pia ilieleza kuwa alitumia jiwe kupasua mifupa ili kurahisisha utupaji wa mabaki.

Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Geoffrey Mwakasenge ulipinga hukumu hiyo, ukidai kuwa mahakama haikuzingatia ipasavyo masuala muhimu yakiwemo ramani ya eneo la tukio, utaratibu wa uchunguzi wa DNA pamoja na hali ya akili ya mshtakiwa.

READ  Huduma zarejea Dubai Airport

Mahakama ilisimama na uamuzi wake ikieleza kuwa ushahidi uliwasilishwa ulikidhi viwango vya kisheria vinavyotakiwa na hivyo kutoa adhabu ya kunyongwa.