Jeshi la majini la El Salvador limekamata meli iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Tanzania, yenye usajili wa Zanzibar, baada ya kubainika kubeba tani 6.6 za dawa za kulevya aina ya cocaine katika operesheni ya baharini.
Meli hiyo yenye urefu wa takribani mita 54, iliyotajwa kama FMS Eagle, ilikamatwa umbali wa takribani maili 380 za baharini kusini-magharibi mwa pwani ya Pasifiki ya El Salvador. Kwa mujibu wa mamlaka za nchi hiyo, mizigo 330 ya cocaine iligunduliwa ikiwa imefichwa ndani ya matangi ya maji ya kusawazisha uzito wa meli (ballast tanks). Thamani ya mzigo huo inakadiriwa kufikia dola milioni 165 za Marekani.
Rais wa El Salvador, Nayib Bukele, alisema tukio hilo ni ukamataji mkubwa zaidi wa dawa za kulevya kuwahi kufanywa na nchi hiyo. Picha na video zilizotolewa na jeshi la majini zinaonyesha vifurushi vya dawa hizo vikiwa vimepangwa juu ya staha ya meli baada ya operesheni.
Watu kumi waliokuwa kwenye meli hiyo walikamatwa, wakiwa ni raia wa mataifa mbalimbali ikiwemo Colombia, Nicaragua, Panama na Ecuador. Hakuna taarifa ya kuwapo kwa raia wa Tanzania miongoni mwa waliokamatwa.
Kwa upande wa Tanzania, msemaji wa serikali, Gerson Msigwa, alisema meli hiyo ilikuwa imesajiliwa Zanzibar na ilikuwa ikipeperusha bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kukamatwa kwake. Hata hivyo, alifafanua kuwa meli hiyo ilikuwa inamilikiwa na wageni na haikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na shughuli za kitaifa za Tanzania.
Msigwa alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua ya kuifuta meli hiyo kwenye daftari la usajili na imeanza mchakato wa kuchunguza umiliki wake pamoja na mazingira yaliyopelekea kuhusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu matumizi ya usajili wa meli katika nchi mbalimbali, ambapo baadhi ya vyombo vya usafiri wa baharini husajiliwa katika mataifa tofauti na yale yanayomilikiwa au kuendeshwa kibiashara.
Mamlaka za El Salvador zinaendelea na uchunguzi kubaini safari ya meli hiyo ilikotoka na ilikokuwa ikielekea, pamoja na mtandao mpana unaohusishwa na shehena hiyo ya dawa za kulevya.




