Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini mkoani Lindi, Selemani Said Bungara maarufu kwa jina la “Bwege,” amefariki dunia akiwa katika matibabu katika hospitali binafsi iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.
Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na kaka yake, Abbas S.A. Bungara, aliyesema marehemu alifikishwa hospitalini hapo kwa ajili ya kuendelea na matibabu ya kuchuja figo (dialysis) kabla ya hali yake kuzorota.
Amesema kwa sasa taratibu za mazishi zinaendelea, huku familia ikiwa imepokea waombolezaji nyumbani kwake Temeke jijini Dar es Salaam.
Bungara atakumbukwa kama mwanasiasa aliyekuwa na msimamo mkali na sauti ya wazi, akijijengea umaarufu ndani na nje ya majukwaa ya kisiasa.
Safari yake ya kisiasa ilipitia vyama tofauti vya upinzani. Aliwahi kuwa mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), baadaye akajiunga na ACT Wazalendo, na hivi karibuni alitangaza kuhamia CHADEMA.
Mabadiliko hayo ya vyama yalikuja katika kipindi ambacho upinzani nchini ulikuwa unapitia migawanyiko ya ndani, hasa baada ya migogoro iliyoathiri CUF na kusababisha kuibuka kwa makundi mapya ya kisiasa.
Katika miaka ya karibuni, Bungara alikuwa akikabiliwa na changamoto za kiafya, ikiwemo matatizo ya figo yaliyomlazimu kupata matibabu ya mara kwa mara ya dialysis.
Pia alipoteza mguu kutokana na maradhi hayo, hali iliyomfanya kutumia kiti cha magurudumu katika kipindi chake cha mwisho cha maisha.
Licha ya hali hiyo, aliendelea kuonekana hadharani. Katika siku zake za mwisho, alihudhuria mara kadhaa vikao vya mahakama kufuatilia kesi inayomhusu mwanasiasa wa upinzani Tundu Lissu.
Bungara aliwahi kulitumikia Jimbo la Kilwa Kusini akiwa chini ya CUF, akijulikana kwa ukaribu wake na wananchi pamoja na mtindo wake wa kuzungumza bila kificho.
Taarifa zaidi kuhusu ratiba ya mazishi zinatarajiwa kutolewa na familia.








